Nuru ya Kiswahili https://nuru.udom.ac.tz/index.php/journal1
Nuru ya Kiswahili is an international peer-reviewed journal that aims to publish theoretical and empirical studies that contribute to our understanding of Swahili language, linguistics and literature. We accept manuscripts written in both Swahili and English languages.
The University of Dodoma en-US Nuru ya Kiswahili 2714-1969 Mtazamo kuhusu Wakati katika Falsafa ya Kiafrika: Mifano kutoka Riwaya Teule za Kiswahili https://nuru.udom.ac.tz/index.php/journal1/article/view/27
Waafrika kama zilivyo jamii nyinginezo duniani wana falsafa inayoongoza maisha yao. Katika uga wa fasihi, wataalamu mbalimbali wametafiti na kuangalia namna falsafa hiyo inavyodhihirika kupitia vipengele mbalimbali vya maisha. Hata hivyo, mtazamo kuhusu wakati kama kipengele kinachoibua Falsafa ya Waafrika, kwa kuhusisha udhihirikaji wake na vipengele vingine vya kifalsafa hakijamakinikiwa vya kutosha. Jambo hili linasababisha ufinyu wa mawanda katika kuelewa mtazamo wa falsafa ya wakati, uhusiano wake na vipengele vingine vya kifalsafa pamoja na athari zake kwa jamii ya Waafrika. Kwa kuzingatia pengo hilo la kimaarifa, makala hii imekusudiwa kubainisha mtazamo kuhusu wakati kwa Waafrika kama unavyodhihirika kupitia vipengele mbalimbali vya kifalsafa pamoja na athari zake kwa jamii. Data za makala hii zilikusanywa maktabani na uwandani. Nadharia ya Ontolojia ya Kiafrika ilitumika katika uchanganuzi na uwasilishaji wa matokeo ya utafiti. Kwa ujumla, makala inabainisha kuwa mtazamo kuhusu wakati ni kipengele muhimu sana kwa Waafrika kwani una athari kubwa kwa namna wanavyoyaendesha maisha yao. Waafrika wanaamini kuwa wakati ni kiini cha ‘kuwapo’ kwa mwanadamu kunakojibainisha kupitia vipengele mbalimbali katika maisha kama vile uzazi, maisha baada ya kifo pamoja na busara na hekima ambazo huaminika kuwapo kwa wazee walio hai pamoja na waliokufa.
Stella Faustine Copyright (c) 2024 Nuru ya Kiswahili 2023-12-31 2023-12-31 2 2 1 24 Ufundishaji wa Kiswahili kama Lugha ya Pili kupitia Fasihi https://nuru.udom.ac.tz/index.php/journal1/article/view/23
Elimu ya Rwanda inakabiliwa na changamoto ya kikwazo cha lugha, hasa lugha ya kufundishia. Walimu wanasema kuwa mara nyingi wanafunzi hushindwa kuelewa masomo kutokana na kiwango kidogo cha uelewa na kuwasiliana katika lugha wanazojifunza shuleni (Urunana, 2018). Hali hii imetoa msukumo wa kuibuka kwa makala hii ili kutathmini namna fasihi inavyotumiwa, na inavyoweza kutumiwa katika ufundishaji wa lugha ya pili kwa mazingira yanayotawaliwa na mtaala wa umahiri nchini Rwanda. Utafiti ulioibua makala hii uliegemea katika mkabala wa kitaamuli na kuongozwa na Nadharia Jengaji iliyioasisiwa na Piaget kati ya miaka 1896 – 1980. Mbinu za ukusanyaji data zilizotumika ni mahojiano, ushuhudiaji na uchambuzi matini. Kwa kutumia sampuli lengwa, washiriki wa utafiti walikuwa walimu kumi na tano (15) na wanafunzi sabini (70) wa Kiswahili kutoka shule za sekondari nne zilizochaguliwa nchini Rwanda. Matokeo ya utafiti yanaonesha kuwa fasihi huchukuliwa kama somo tu. Walimu na wanafunzi hawajatambua kwamba fasihi inaweza kutumiwa kama nyenzo ya kufundishia na kujifunzia lugha na hawajajua namna ya kuitumia.
Donard Bikorimana Copyright (c) 2024 Nuru ya Kiswahili 2023-12-31 2023-12-31 2 2 25 48 Ruwaza ya Vitenzi vya Kibantu katika Muktadha wa Vitenzi vya Kiswahili https://nuru.udom.ac.tz/index.php/journal1/article/view/29
Makala hii inahusu ruwaza ya vitenzi vya Kibantu katika muktadha wa vitenzi vya Kiswahili. Lengo la makala hii ni kuonesha utokeaji wa viambishi vya ruwaza ya vitenzi vya Kibantu katika Kiswahili iwapo vinajitokeza vyote au la na matumizi ya viambishi hivyo katika Kiswahili. Hili linasaidia kuongeza zaidi maarifa katika mofolojia ya Kiswahili na kuendelea kuthibitisha Ubantu wa Kiswahili.  Lengo hilo limetimizwa kwa kutumia data ya mifano ya vitenzi vyenye viambishi mbalimbali vilivyokusanywa katika baadhi ya vitabu vya mofolojia ya Kiswahili.  Kwa hiyo, kutokana na mifano hiyo ya vitenzi vilivyochanganuliwa kwa kutumia mhimili wa kufuta mabano wa Nadharia ya Mofolojia Leksika, yafuatayo yamebainika: Kiswahili kinabeba viambishi vingi vya ruwaza ya vitenzi vya Kibantu, isipokuwa viambishi vichache ambavyo havidhihiriki kabisa katika Kiswahili. Viambishi hivyo ni kama viambishi awali tangulizi vya uwakilishi. Pamoja na hayo, kuna baadhi ya viambishi vya ruwaza hiyo vinavyotokea katika Kiswahili vikiwa na mazingira maalumu ya utokeaji wake kama kiambishi tamati tangulizi na baadhi ya viambishi tamati vya ziada. Kwa hiyo, kiambishi tamati tangulizi na baadhi ya viambishi tamati vya ziada vinaweza kuchunguzwa zaidi. Hii itasaidia kuona mazingira mbalimbali ya utokeaji wa baadhi ya viambishi hivyo katika Kiswahili.
Johari Hakimu Copyright (c) 2024 Nuru ya Kiswahili 2023-12-31 2023-12-31 2 2 49 73 Sifa za Hofu katika Maisha ya Mwanadamu https://nuru.udom.ac.tz/index.php/journal1/article/view/35
Kila mwanadamu mwenye uwezo wa kufikiri na kutafakari juu ya masuala mbalimbali yanayomzunguka huonesha hisia zinazoambatana na hali fulani katika kutoa maamuzi ya tafakuri yake. Moja kati ya hali zinazotawala fikra zake ni hofu. Kuwapo kwa hofu hubainika kupitia matendo ayafanyayo katika mazingira yanayomzunguka. Kimsingi, hofu humwongoza mwanadamu kuwa na maamuzi yanayosababisha kufanya au kutofanya jambo fulani. Kazi za kibunilizi, mathalani riwaya husawiri maisha halisi ya mwanadamu yanayofungamana na hali mbalimbali, ikiwamo hofu. Kwa msingi huo, makala hii inabainisha sifa za hofu kwa kumrejelea mhusika Ngoma kutoka riwaya ya Ua la Faraja. Data zilipatikana maktabani kwa kutumia mbinu ya usomaji matini. Vilevile, mbinu ya usaili ilitumika ili kupata data za kuthibitisha uhalisi wa sifa za hofu katika ulimwengu halisi wa mwanadamu. Misingi ya Nadharia ya Uhalisia imetumika katika uchunguzi, uchanganuzi na uwasilishaji wa matokeo ya utafiti. Matokeo ya utafiti huu yanaonesha kuwa katika riwaya ya Ua la Faraja kuna sifa kuu tatu za hofu: hofu hujizalisha kulingana na wakati, hofu huhusisha mlolongo wa wahusika wenye nasaba na hofu huibua tabia mpya kwa mwanadamu.
Martina Duwe Copyright (c) 2024 Nuru ya Kiswahili 2023-12-31 2023-12-31 2 2 74 102